Pixabay
18 Feb 2021 Toleo la habari Ecosystems and Biodiversity

Ripoti mpya sanisi ya UNEP, inazungumzia kwa kina umuhimu wa kutatua changamoto za sayari ili kuwa na hatima bora

  • Mkutano unaozungumzia mazingira na malengo ya bayoanuai, kupunguza mno uchafuzi na kufikia matakwa ya SDGs ili kuwezesha maendeleo endelevu katika jamii
  • Kubadili mielekeo yetu na kufanya mazingira nguzo wakati wa kufanya maamuzi makuu ili kuwa na mabadiliko ya kudumu
  • Mikakati ya kuimarisha uchumi baada ya COVID-19 ni fursa mwafaka ya kuwekeza kwa mazingira na kukomesha uzalishaji wa gesi chafu kufikia mwaka wa 2050

Nairobi, Februari 18, 2021 – Dunia inaweza kubadili uhusiano wake na mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai na uchafuzi kwa wakati mmoja ili kuwa na hatima endelevu na kuzuia uwezekano wa kutokea kwa magonjwa tandavu katika siku zijazo, kwa mjibu wa ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inayozungumzia kwa kina jinsi ya kushughulikia kwa dharura changamoto za mazingira zinazojitokeza kwa njia tatu.

Ripoti hiyo, Kufanya Amani na Mazingira, inaonyesha kiwango cha changamoto hizi kwa mazingira kwa kutoa mafunzo kupitia tathmini za kimataifa, ikijumuisha zile kutoka kwa Jopo la Kimataifa Kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi na Jukwaa la Kimataifa la Sera ya Sayansi ya Bayoanuai na Huduma za Mifumo ya Ekolojia, pamoja na ile ya UNEP ya ripoti ya Hali ya Mazingira Duniani, Jopo la UNEP la Rasilimali za Kimataifa, na matokeo mapya ya utafiti kuhusu kuzuka kwa  magonjwa kutoka kwa wanyama kama vile COVID-19.

Waandishi wanatathmini uhusiano uliopo kati ya changamoto anuai za mazingira na za maendeleo, na kueleza jinsi ambavyo kukua kwa sayansi na kuunda sera dhabiti kunaweza kusaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu kufikia mwaka wa 2030 na kukomesha uzalishaji wa gesi chafu kufikia mwaka wa 2050 huku kukiwa na upunguzaji wa uharibifu wa bayoanuai, uchafuzi na taka. Hiyo itamaanisha ubunifu na uwekezaji kwenye shughuli pekee zinazotunza watu na mazingira. Mafanikio yatajumuisha uboreshaji wa mifumo ya ekolojia, maisha mazuri na mazingira dhabiti.

"Kwa kutumia ushahidi kutoka katika tafiti za hivi karibuni zinazoonyesha athari na madhara yanayotokea kwa mazingira kwa dharura, changamoto za bayoanuai na uchafuzi unaopelekea vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka, [ripoti hii] inaonyesha wazi kuwa vita vyetu dhidi ya mazingira vimeyaharibu," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema katika dibaji ya ripoti hiyo. "Pia inatuelekeza mahali salama kwa kuweka mikakati ya amani na programu ya ujenzi mpya baada ya vita.

"Kwa kubadilisha mielekeo yetu kuhusu mazingira, tunaweza tukatambua umuhimu wake. Kwa kuunda sera, mikakati na mifumo ya kiuchumi inayoonyesha kuwa tunathamini mazingira, tunaweza kuwekeza kwenye shughuli za kuboresha mazingira na kutuzwa," aliongezea.  "Kwa kutambua kuwa mazingira ni mshirika mwenza, tunaweza kuonyesha uwezo wa binadamu wa kutatua masuala changamano ili kuwa na maendeleo endelevu na kuwa na afya njema na mazingira bora."

Wakati uwekezaji wa kuimarisha chumi zilizoathiriwa na janga la COVID-19 unapoendelea, ripoti hiyo ya kina inaonyesha fursa na udharura wa kuchukua hatua dhabiti kwa haraka. Pia inaonyesha wajibu wa kila mmoja – kuanzia kwa serikali na mashirika ya biashara hadi kwa jamii na watu binafsi – wanaweza na ni sharti wautekeleze. Mwaka wa 2021 ni muhimu mno, tunapoelekea mikutano ya mazingira na bayoanuai  - UNFCCC COP 26 na CBD COP 15 – ambapo serikali zinahitaji kuweka malengo makuu kwa ushirikiano ili kutunza mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu takribani maradufu katika karne hii, na kwa kutunza na kuboresha bayoanuai.

Kukabiliana na changamoto za sayari zinazojitokeza kwa njia tatu

Ukuaji wa uchumi umesababisha ustawi unaotofautiana kwa idadi ya watu inyoongezeka kwa kasi duniani, na kufanya watu bilioni 1.3 kuwa maskini, hukuuchimbaji wa malighafi ukiongezeka mara tatu na kufikia viwango hatari na kusababisha hali ya dharura duniani. Ijapokuwa uzalishaji wa gesi chafu ulipungua kutokana na ugonjwa mtandavu, dunia  inaelekea kufikisha angalau nyuzijoto 3 kutokana na ongezeko la joto kwenye karne hii; zaidi ya milioni 1 ya takribani spishi milioni 8 za mimea na wanyama zimo hatarini kuangamia; na magonjwa kutokana na uchafuzi yanapelekea takribani vifo vya watu milioni 9 wanaokufa mapema kila mwaka. Uharibifu wa mazingira ni kuzingiti kwa ukomeshaji wa umaskini na baa la njaa, kupunguza kutokuwa na usawa na kuwezesha uchumi kukua kwa njia endelevu, kila mtu kuwa na ajira na kuwa na jamii zilizo amani zisizo na ubaguzi.

Ripoti hii inaonyesha jinsi changamoto hizi za mazingira zinazojitokeza kwa njia tatu huungiliana na kusababishwa na vyanzo vilevile, zinanaweza tu kushughulikiwa kwa pamoja kikamilifu. Ruzuku kwa fueli ya visukuku, kwa mfano, na bei ya bidhaa bila kujumuisha mazingira, huongoza uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia inayoharibu nishati na malighafi na ndicho chanzo cha changamoto zote tatu.

Inger Andersen, Katibu Mtendaji wa UNEP, alisema kuwa ripoti hiyo ilionyesha umuhimu wa kubadilisha mielekeo yetu na mambo tunayothamini, na kutafuta masuluhisho ya kisiasa na kiufundi ya kukabiliana na changamoto za Mazingira.

"Kwa kuonyesha jinsi ambavyo afya ya binadamu na hali ya mazingira vinavyoingiliana, janga la COVID-19 limeonyesha umuhimu wa kubadilisha mienendo yetu kuhisiana na mazingira. Kwa kujumuisha mambo tunayithamini wakati wa kufanya uamuzi – iwe sera ya kiuchumi au uamuzi ya mtu binafsi – tunaweza kusababisha mabadiliko makuu ya kudumu yatakayowezesha uendelevu wa binadamu na mazingira," alisema. “Mikakati ya ‘Green recovery’ kwa chumi zilizoathiriwa na ugonjwa mtandavu ni fursa kuu ya kuleta mabadiliko kwa haraka."

Ripoti iliotolewa tunapoelekea kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa, ripoti hii inaonyesha ni kwa nini hatua za dharura zinahitajika ili kutunza na kuboresha sayari na mazingira yake kwa jumla.

Inatoa mifamo ya mabadiliko ya kudumu na jinsi yanavyoweza kustawisha kukuza ajira na kusababisha usawa zaidi. Mabadiliko makuu yanajumuisha kuchunguza upya jinsi tunavyothamini na kuwekeza kwa mazingira, kupitia kwa sera na uamuzi katika ngazi zote, kubadilisha ruzuku na vipengele vinginevyo vya mifumo ya uchumi na fedha, na kukuza ubunifu wa teknolojia endelevu na mifumo endelevu ya biashara. Uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi kwenye vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme na fueli mbadala inaonyesha jinsi ambavyo sekta mbalimbali zimetambua manufaa ya kuleta mabadiliko haraka.

Waandishi wanaeleza kuwa kukomesha uharibifu wa mazingira kwa njia zote zinazoshuhudiwa ni muhimu ili kufikia mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, hasa kukomesha umasikini, kuhakikisha kuna chakula na maji ya kutosha na siha njema kwa wote. Mfano mzuri ni jinsi ambavyo kuimarishwa kwa kilimo na uvuvi na kuvifanya endelevu, ikijumuishwa na mabadiliko ya lishe na kupunguza uharibifu wa chakula, vinaweza kupunguza baa la njaa na umaskini duniani na kuboresha lishe na afya huku ardhi zaidi na bahari vikitengewa mazingira.

Kuimarisha wito wa kuchukua hatua, ripoti hiyo inasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kushirikisha wadau katika ngazi zote katika jamii wakati wa kufanya maamuzi, na kutoa hatua kuu ambazo serikali, mashirika ya biashara, jamii na watu binafsi wanaweza na wanapaswa kuteleza ili kuwa na maendeleo endelevu duniani.

Kwa mfano:

  • Serikali zinaweza kujumuisha kodi ya mtaji kwenye mikakati ya kukuza uchumi, kuwekea gharama kaboni na kupunguza ruzuku ya trilioni za dola kwa fueli ya visukuku, kilimo kisicho endelevu na usafiri na kutumia ruzuku hizo kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa na masuluhisho yanayojali mazingira
  • Mashirika ya kimataifa yanaweza kukuza mbinu ya "One Health" na kuweka malengo mapana ya bayoanuai, kama vile kuongeza mitandao ya maeneo yanayotunzwa
  • Mashirika ya kifedha yanaweza kuacha kutoa mikopo ya nishati ya visukuku na kukuza ufadhili bunifu ya utunzaji wa bayoanuai na kilimo endelevu.
  • Mashirika ya biashara yanaweza kuweka mikakati ya kukuza uchumi unategemea matumizi ya bidhaa zilizotumika kuunda bidhaa zingine na kupunguza matumizi ya rasilimali na uharibifu na kujitolea kufanya mambo kwa uwazi kwenye mifumo ya usambasaji
  • Mashirika Yasiyokuwa ya serikali yanaweza kubuni mitandao ya wadau ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu wakati wa maamuzi kuhusu matumizi endelevu ya ardhi na rasilimali za baharini
  • Mashirika ya kisayansi yanaweza kuanzisha teknolojia na sera za kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, kuimarisha matumizi ya rasilimali na kuimarisha miji, viwanda, jamii na mifumo ya ekolojia.
  • Watu binafsi wanapaswa kuchunguza upya ushirikiano wao na mazingira, wajielimishe kuhusu uendelevu na kubadili mienendo yetu ili kupunguza matumizi yao ya rasilimali, kupunguza uharibifu wa chakula, wa maji na nishati na kutumia lishe bora.

Hatima endelevu inamaanisha pia kupata funzo kutoka kwa janga la COVID-19 ili kupunguza uwezekano wa ugonjwa mwingine mtandavu kutokea. Ripoti hii inaonyesha kuwa uharibifu wa mifumo ya ekolojia unaongeza uwezekano wa vimelea vya kuambukizwa magonjwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu, na umuhimu wa mbinu ya ‘One Health’ inayozingatia afya ya watu, wanyama na binadamu kwa wakati mmoja.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira anayeweka ajenda ya kimataifa ya mazingira. UNEP hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA)

UNEA ni tasisi ya ngazi ya juu zaidi duniani inayotoa uamuzi kuhusiana na masuala ya mazingira. Baraza la Mazingira hukutana mara mbili kwa mwaka kuainisha masuala muhimu ya kujumuishwa sera na kuunda sheria za kimataifa kuhusiana na mazingira. Kupitia maazimio yake na wito wa kuchukua hatua, Baraza hilo hutoa uongozi na kuchombea ushirikiano wa nchi kuchukua hatua za kushughulikia mazingira.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa