04 Jun 2021 Toleo la habari Ecosystems and Biodiversity

Buni, Tafakari, Boresha! Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia wazinduliwa

Juni 4, 2021, Nairobi/Roma – Viongozi kote ulimwenguni katika nyanja za kisiasa, sayansi, jamii, dini na tamaduni walijumuika leo ili kuzindua rasmi Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia - wito wa kuhamasisha kuhusu uboreshaji wa mamilioni ya hekta ya mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni kwa manufaa ya watu na sayari.

Ukiongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Muongo wa Uboreshaji - utakaodumu kuanzia mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2030 - uliidhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kupitia azimio la mwaka wa 2019.

Uzinduzi uliofanyika kwenye hafla mtandaoni ulijumuisha viongozi wa ngazi za juu, pamoja na viongozi wa UNEP na FAO na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan, mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni mwaka huu; Papa Francis; Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika; Kansela wa Ujerumani Angela Merkel; na Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley. Miongoni mwa watu maarufu katika ngazi ya kimataifa waliozungumza ni pamoja na Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa Jane Goodall na mabalozi wengine wa nia njema, mawakili, wawakilishi wa vijana, wanasayansi na CEOs.

"Kwa kuboresha mifumo ya ekolojia, tunaweza kuleta mabadiliko ambayo yatachangia kufanikisha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Kazi ni nyingi. Tunahitaji kupanda tena miti na kutunza misitu yetu. Tunahitaji kusafisha mito na bahari zetu. Na tunahitaji kupanda miti mijimi mwetu," Katibu Mkuu wa UN alisema katika ujumbe wake. "Kwa kufanya mambo haya hatutaweza tu kutunza rasilimali kwenye sayari. Pia, tutazalisha mamilioni ya kazi mpya kufikia mwaka wa 2030, kujipatia mapato ya zaidi ya dola trilioni 7 kila mwaka na kusaidia kukomesha umaskini na baa la njaa.”

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu, alisema kuwa shinikizo linalozidi kuongezeka na kuwekwa kwa malighafi ulimwenguni linaathiri maisha ya asilimia 40 ya jumla ya idadi ya watu ulimwenguni, alitoa wito wa kubadili mienendo yetu.

"Hatuwezi kuendelea na mambo kama kawaida!" alisisitiza. “Tunahitaji kuzuia, kusitisha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, ikijumuisha mashamba yetu na misitu; mito na bahari zetu . Mifumo ya kilimo cha chakula dhabiti yenye ufanisi zaidi, na endelevu inaweza kusaidia kuboresha mifumo ya ekolojia na kuwezesha kuzalisha chakula kwa njia endelevu, bila kuacha mtu nyuma, ”aliongezea.

"Ni sharti tutumie fursa hii katika historia kuzindua vuguvugu kubwa la kimataifa ili kuokoa mifumo yetu ya ekolojia ya nchi kavu na bahari hata tunapoendelea kupunguza gesi ya ukaa. Kila mtu ana 'wajibu wa kutekeleza' hapa," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen. “Serikali ni sharti zihakikishe pesa zinazotengewa kujiimarisha baada ya COVID-19 zinachangia kujiimarisha kwa njia endelevu na bila ubaguzi. Mashirika ya biashara na sekta za kifedha lazima zibadilishe jinsi zinavyofanya kazi na matumizi ya fedha ili kuboresha dunia silia. Na kama watu binafsi na watumiaji wa bidhaa, ni wakati wa kutafakari kuhusu maamuzi yetu, kuitisha bidhaa zisizosababisha ukataji wa miti na kupigania uendelevu. ”

"Kuboresha mazingira tuliyoharibu kunamaanisha, kwanza, kujirekebisha," alisema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa video uliotumwa na Kardinali Pietro Parolin, Waziri wa Mambo ya Nje. "Tunakaribisha Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, tuwe wachangamfu, wabunifu na ujasiri. Na tuchukue nafasi yetu inayofaa kama 'Kizazi cha Uboreshaji'"

Muongo huu unakusudia kuhamasisha na kusaidia serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya uraia, kampuni za sekta binafsi, vijana, vikundi vya wanawake, watu wa kiasili, wakulima, jamii za wenyeji na watu binafsi kote ulimwenguni, kushirikiana, kukuza na kuchochea mradi ya uboreshaji ulimwenguni. Jitihada zitahusisha shughuli nyingi. Ni pamoja na kuweka ruzuku kwenye bajeti na kutenga fedha za kukuza uboreshaji, kufanya utafiti kuhusu uboreshaji wa mazingira ya nchi kavu na baharini, kujengea wanaohusika na uboreshaji kote ulimwenguni uwezo wa kiufundi na kufuatilia maendeleo ya uboreshaji kote ulimwenguni.

Muongo huu unakusudia kuhamasisha mamia ya mamilioni ya watu kuboresha mazingira na kukuza utamaduni wa uboreshaji kote ulimwenguni ambapo miradi ya uboreshaji itaimarishwa kote ulimwenguni.

“Dunia haina budi ila kutunza mazingira kwa njia nzuri, hali ambayo haitaimarisha tu uchumi ila pia kutunza mazingira," alisema Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan, ambaye nchi yake katika mwaka wa 2019 ilianzisha mpango kabambe wa kupanda miti bilioni 10.

Akikaribisha kuzinduliwa kwa Muongo wa Umoja wa Mataifa, Felix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika, alisema kuwa bara la Afrika limejitolea kwa njia nyingi kupitia Maazimio kadhaa ya kikanda, ahadi, Wito wa Kuchukua Hatua na miradi ya majaribio, ila kuna haja ya kukusanya rasilimali zote zinazohitajika na wataalam wanaohitajika ili kuwezesha utekelezaji mkubwa.

"Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ya nchi kavu, ya baharini na maji safi unapaswa kufanywa kwa njia ya kuzuia kuzuka kwa migogoro ya ardhi au migogoro ya matumizi yake," akaongezea. "Kwa hivyo lazima iwe sehemu ya upangaji wa michakato ya anga kwa kuzingatia ni kipi kinachoweza kupotezwa kati ya sekta, kuheshimu haki za umiliki wa ardhi na rasilimali za jamii na vikundi vingine vya kijamii vilivyo hatarini."

Katika ujumbe wake, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema: "Ni sharti tuchukue hatua zaidi kutunza na kuboresha makazi ya asili - na lazima tufanye hivyo sasa, wala sio wakati ujao."

"Lazima sasa tuhakikishe kwamba misitu, ambayo hatuhitaji mno ili kudhibiti hali ya hewa yetu, inatunzwa na kukuzwa tena," aliongezea.

Kansela huyo pia alitangaza kuwa Ujerumani itakuwa nchi ya kwanza kutoa ufadhili - Yuro milioni 14 - kwa Mfuko wa Wakfu wa Wabia Anuai (Multi-Partner Trust Fund) wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia

Uzinduzi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia leo unatuelekeza kwenye Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 mwezi wa Juni, siku kuu ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha ulimwengu uchukue hatua za kushughulikia mazingira. Uzinduzi uliyofanyika chini ya kaulimbiu ya uborejeshaji wa mifumo ya ekolojia, Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu imeandaliwa na Pakistani, ambayo itasherehekea siku hii na kuzindua Muongo wa UN kupitia hafla inayofanyika Islamabad na kuongozwa na Waziri Mkuu Imran Khan. Washiriki watajumuisha waheshimiwa wengi kutoka pembe zote za dunia ikijumuisha Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen na maafisa wakuu wa FAO, UN-Habitat na UNDP, pamoja na maafisa wakuu kutoka kwa nchi zikiwemo Ujerumani na Saudi Arabia.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

 Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 unatoa wito wa kutunzwa na kuboreshwa kwa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, kwa manufaa ya watu na mazingira.  Unalenga kukomesha uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na kuiboresha ili kufikia malengo ya kimataifa. Baraza la Umoja wa Mataifa limetangazaMuongo wa Umoja wa Mataifa na unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Muongo wa Umoja wa Mataifa unaunda vuguvugu dhabiti lenye msingi mpana wa kimataifa ili kuimarisha uboreshaji na kuiwezesha dunia kuwa na hatima endelevu. Hiyo itajumuisha kuimarisha uwezo wa kisiasa wa uborejeshaji na maelfu ya miradi inayoendelea.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

 Kuhusu Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ni shirika maalum la Umoja wa Mataifa linaloongoza juhudi za kimataifa za kutokomeza baa la njaa na kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula kwa kuifanya kuwa dhabiti zaidi, endelevu na isiyobagua.  Lengo la FAO ni kuwa na utoshelezaji wa chakula kwa watu wote na kuhakikisha kuwa watu wanapata chakula cha hali ya juu cha kutosha mara kwa mara ili kuwa na maisha mazuri, na watu wenye afya. 

Kuhusu Siku ya Mazingira Duniani

Siku inayoadhimidhwa kila tarehe 5 mwezi wa Juni, Siku ya Mazingira Duniani ni siku kuu ya Umoja wa Mataifa inayoadhimishwa kila mwaka kuhamasisha dunia kuhusu umuhimu wa kutunza sayari yetu.

Mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2021 ni Pakistani chini ya kaulimbiu ya "Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia" kupitia kampeni ya "Tafakari. Buni.  Boresha." Mwaka huu, Siku hiyo pia itatumika kama uzinduzi rasmi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030. Hashtagi rasmi za Siku hiyo ni #GenerationRestoration na #SikuTaMazingiraDuniani. Maadhimisho kote ulimwenguni yanajumuisha shughuli mtandaoni na hafla za ana kwa ana. 

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

 

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP

Irina Utkina, Ofisa wa Uhusiano Mwema (Roma), FAO (+39) 06 570 52542,

 

 

 

Maudhui yanayokaribiana